Taarifa kwa Umma: Chanjo za VVU zilizojaribiwa katika utafiti wa PrEPVacc zashindwa kupunguza maambukizi

*Powerpoint slides presented at AIDS 2024 here*

Chini ya Embargo kuelekea

 

Jumanne tarehe 23 Julai 2024

06:00 Mchana

 

Chanjo za VVU zilizojaribiwa katika utafiti wa PrEPVacc zashindwa kupunguza maambukizi

 

Matokeo ya jaribio la chanjo ya VVU la PrEPVacc lililofanywa Mashariki na Kusini mwa Afrika, ambalo lilifanyika kati ya mwaka 2020 na 2024, yanaonyesha bila shaka kuwa kati ya aina mbili za chanjo zilizojaribiwa hakuna iliyopunguza maambukizi ya VVU kwa washiriki wa utafiti.

Chanjo kwenye jaribio la PrEPVacc zilisitishwa mnamo Novemba 2023 (na kutangazwa hadharani mnamo Desemba 2023) ilipobainika wazi kwa wataalam huru waliofuatilia data ya utafiti kwamba kulikuwa na uwezekano mdogo au hakuna uwezekano kabisa wa chanjo kuonyesha ufanisi katika kuzuia maambukizi ya VVU.

Matokeo ya majaribio ya chanjo ya PrEPVacc, yaliyotangazwa katika Kongamano la UKIMWI 2024 huko Munich, Ujerumani, yanaripoti maambukizi zaidi katika makundi mawili ya chanjo kuliko kundi la kipozaungo, lakini watafiti wanasema hawawezi kupata hitimisho la uhakika juu ya hii inamaanisha nini kwa sababu  kitakwimu inaonyesha mlinganisho ni mpana sana, kuashiria kiwango cha juu cha kutokuwa na uhakika.

Watafiti pia wana angazia kwamba kiwango cha maambukizi ya VVU kilichoonekana katika kundi la kipozaungo kilikuwa cha chini isivyo kawaida na haionekani kuelezewa na tofauti katika matumizi ya kondomu au dawakinga.

PrEPVacc inajadili na makundi mengine duniani kote kwa uchanganuzi zaidi wa chanjo ambao unaweza kusaidia kueleza tofauti za viwango vya maambukizi ya VVU kati ya makundi ya chanjo na kipozaungo.

Kote Afrika Kusini, Tanzania na Uganda, nchi ambazo majaribio ya PrEPVacc yamefanyika, mpango wa umoja wa mataifa kuhusu ukimwi (UNAIDS) unakadiria kuwa mnamo mwaka 2022, jumla ya watu milioni 10.7 walikuwa wanaishi na VVU, watu wazima na watoto 244,000 waligunduliwa kuwa na VVU. Wakati washiriki wa utafiti wa PrEPVacc walipotoka kwenye utafiti, PrEPVacc lilikuwa jaribio pekee linaloendelea la ufanisi wa chanjo ya VVU duniani, na kwa sasa hakuna majaribio mengine ya ufanisi wa chanjo ya VVU yanayoendelea au yanayotarajiwa. PrEPVacc ni jaribio la kwanza la ufanisi wa chanjo ya VVU kufanywa katika nchi za Afrika Mashariki.

Utafiti wa PrEPVacc ni majaribio matatu katika moja, unaoongozwa na watafiti wa Kiafrika kwa usaidizi kutoka kwa washirika wa Ulaya,. Katika majaribio yake ya ufanisi wa utafiti wa awamu ya IIb, ilijaribu dawa mbili tofauti za chanjo ili kuona kama mojawapo inaweza kuzuia maambukizi ya VVU kwa watu ambao wanaweza kuwa katika hatari ya kupata VVU. Katika kipindi ambacho washiriki walipata chanjo tatu za kwanza, aina mpya ya dawakinga pia ilifanyiwa majaribio dhidi ya dawakinga zilizopo kwenye huduma ili kuona kama ilikuwa na ufanisi katika kuzuia maambukizi ya VVU. Matokeo ya utafiti wa dawakinga ni tofauti na matokeo ya chanjo na yatatangazwa baadaye mwaka huu 2024.

Mtazamo wa utafiti kwa ufupi

Katika vituo vinne vilivyoshiriki utafiti huko Masaka, Uganda; Mbeya na Dar es Salaam, Tanzania; na Durban, Afrika Kusini, PrEPVacc iliandikisha washiriki watu wazima 1,512 wenye afya njema wenye umri wa miaka 18-40 ambao waliripoti tabia zinazowafanya kuwa katika hatari zaidi ya kupata VVU. Kituo cha Masaka na Durban viliandikisha wanaume na wanawake, na kituo cha Mbeya na Dar es Salaam viliandikisha wanawake pekee. Katika vituo vyote, 13% ya washiriki walikuwa wanaume, na 87% walikuwa wanawake.

PrEPVacc ilijaribu michanganyiko miwili tofauti ya chanjo za VVU na ikalinganisha kila moja na kipozaungo (maji ya chumvi) katika ubahatishaji wa 1:1:1. Aina moja ilichanganya chanjo ya DNA (DNA-HIV-PT123) na chanjo ya protini (AIDSVAX B/E), na nyingine ilichanganya chanjo hiyo hiyo ya DNA, kibebeshi cha kirusi kisichogawanyika (MVA-CMDR) na chanjo ya protini. (CN54gp140). Ratiba ya chanjo ilikuwa na mahudhurio manne, mahudhurio matatu yalichukua takriban miezi sita kukamilika na la nne mwaka mmoja baada ya kujiandikisha.

Washiriki wote walipewa ushauri nasaha kuhusu manufaa ya dawakinga katika kipindi chote cha utafiti. Kuanzia uandikishaji hadi wiki mbili baada ya hudhurio lao la tatu la chanjo dawakinga ilitolewa kama mojawapo ya dawa mbili za utafiti, na baada ya hapo, ilitolewa ndani ya nchi katika vituo vingine vinavyotoa huduma ya dawakinga. Zaidi ya hayo, washiriki walipokea ushauri nasaha ulioboreshwa kuhusu hatarya VVU pamoja na taarifa za namna bora ya kujumuisha na kuzingatia matumizi ya dawakinga dhidi ya VVU.

Watafiti wa PrEPVacc walikamilisha jaribio kwa mafanikio, wakitimiza mahitaji ya kimaadili, mikakati ya ushirikiswaji na kutekeleza ushirikishwaji mzuri wa jamii, pia kukamilisha tafiti mbalimali kama sehemu yake ya programu jumuishi ya sayansi ya jamii.

Watafiti walikutana na changamoto katika kutafuta na kuandikisha washiriki kwenye utafiti kipindi cha janga la UVIKO-19 na katika kushughulikia upatikanaji wa chanjo ya MVA. Hili lilishughulikiwa kwa PrEPVacc kubadilisha uwekaji nasibu (randomization) wa washiriki waliojiandikisha kutoka 1:1:1 DNA/AIDSVAX B/E, DNA/MVA-CMDR/CN54gp140 na kundi la kipozaungo, hadi 1:1 kati ya DNA/AIDS VAX B/E na kundi la kipozaungo, na kusitisha uandikishaji kwenye kundi la chanjo ya mchanganyiko wa MVA-CMDR/CN54gp140 katika vituo vyote mnamo Juni 2022.

Uchambuzi wa ufanisi wa chanjo ya msingi ya PrEPVacc uliundwa ili kuzipa chanjo nafasi bora zaidi ya kuonyesha ufanisi kwa kuzingatia tu wale washiriki ambao walipata chanjo tatu au zaidi kutoka kwenye kundi la mchanganyiko wa chanjo au kundi la kipozaungo ambazo ziliwekwa nasibu, ambapo washiriki wote waliochanjwa walitarajiwa kutoa mwitikio wa juu wa kinga.

Idadi ndogo ya maambukizi katika majaribio ya chanjo

Katika uchambuzi wa chanjo ya msingi, kati ya wale waliopata angalau sindano tatu za mchanganyiko wa DNA/AIDSVAX B/E, washiriki 11 kati ya 532 walipata VVU, kiwango cha maambukizi ni 1.73 kwa watu 100 waliofuatiliwa ndani ya mwaka mmoja kila mmoja (takwimu za matukio ya maambukizi mapya) ikilinganishwa na 3 kati ya washiriki 523 waliopokea kipozaungo, kiwango cha maambukizi 0.48 kwa watu 100 waliofuatiliwa ndani ya mwaka mmoja kila mmoja (takwimu za matukio ya maambukizi mapya).

Katika uchambuzi wa msingi wa chanjo, kati ya waliopata mchanganyiko wa MVA-CMDR/CN54gp140, washiriki 9 kati ya 244 walipata VVU, kiwango cha maambukizi 2.38 kwa watu 100 waliofuatiliwa ndani ya mwaka mmoja kila mmoja (takwimu za matukio ya maambukizi mapya) ikilinganishwa na 2 kati ya washiriki 251 waliopokea kipozaungo, kiwango cha maambukizi 0.51 kwa watu 100 waliofuatiliwa ndani ya mwaka mmoja kila mmoja (takwimu za matukio ya maambukizi mapya)

Matokeo haya yanamaanisha kuwa hakuna mchanganyiko wa chanjo uliotoa matokeo yoyote ya ulinzi (kinga), na watafiti wanasema kwamba vipindi vya kupima usahihi wa makadirio ya maambukizi na uwiano wa hatari ni vipana sana hivyo hawawezi kufikia jibu la uhakika kuhusu maana ya idadi kubwa ya maambukizi iliojionyesha kwenye kundi la chanjo.

Kabla ya kutolewa taarifa kwa umma, PrEPVacc imeanzakushiriki matokeo haya na washiriki wa utafiti na jamii ambazo zimekuwa washirika katika jaribio na sasa itawafahamisha washiriki ni kundi gani la chanjo au kipozaungo walilokuwemo katika kipindi cha utafiti.

Hakuna hitimisho la uhakika kutokana na kupata maambukizi zaidi kwenye kundi la chanjo

Kutoka kwenye utafiti wa Kundi la Usajili la PrEPVacc kati ya mwaka 2018 na 2023, kiwango cha maambukizi ya VVU kilikuwa 2.9 kwa watu 100 waliofuatiliwa ndani ya mwaka mmoja kila mmoja (takwimu za matukio ya maambukizi mapya) yalionekana katika vituo vya majaribio ya utafiti wa PrEPVacc. Watafiti wa PrEPVacc wangetarajia kuona matukio sawa ya VVU katika kundi la kipozaungo la majaribio ya chanjo.

Viwango vya maambukizi ya VVU vilivyoonekana vilivyolingana na Makundi ya kipozaungo, vilikuwa 0.48 na 0.51 kwa watu 100 waliofuatiliwa ndani ya mwaka mmoja kila mmoja (takwimu za matukio ya maambukizi mapya), chini sana kuliko ilivyotarajiwa na wachunguzi na kwa vipindi vingi vya kupima usahihi wa makadirio ya maambukizi kulionyesha idadi ndogo ya maambukizi tofauti na ilivyotegemewa na watafiti katika kundi la kipozaungo hii inaongeza wasiwasi.

Kwa kulinganisha, tangazo la hivi majuzi kutoka kwenye utafiti wa PURPOSE 1 wa aina za dawakinga za sindano na za kumeza, ambao ulifanyika katika vituo vitatu vya utafiti nchini Uganda na 25 nchini Afrika Kusini, uliripoti maambukizi 16 kati ya wanawake 1,068 katika kundi lake la dawakinga ya Truvada (matukio ya maambukizi 1.69 kwa watu 100 waliofuatiliwa ndani ya mwaka mmoja kila mmoja) na maambukizi 39 kati ya wanawake 2,136 katika kundi la dawakinga ya Descovy (matukio ya maambukizi 2.02 kwa watu 100 waliofuatiliwa ndani ya mwaka mmoja kila mmoja). Matukio yaliyoripotiwa kwenye utafiti wa PURPOSE 1  yanakaribiana zaidi na yale yaliyotarajiwa katika kundi la kipozaungo la PrEPVacc.

Wakati watafiti wanaona kuwa ni habari njema kwamba matukio ya VVU yalipungua kwa washiriki wa utafiti wakati wa majaribio - kuendelea na mwelekeo ulioonekana katika utafiti wa ufuatiliaji - inamaanisha kuwa kutokuwa na uhakika kuhusu matokeo ya chanjo ya PrEPVacc ni kwingi.

Watafiti hawawezi kuelezea mara moja maambukizi ya chini ya VVU kwenye kundi la kipozaungo. Wameondoa makosa ya takwimu na tofauti katika utumiaji wa dawakinga na kondomu unaoripotiwa na washiriki, na tabia hatarishi kati ya makundi.

Usalama wa chanjo umeonyeshwa katika majaribio ya awali

Washiriki wa chanjo waliojaribiwa katika utafiti wa PrEPVacc wametathminiwa katika michanganyiko mbalimbali kwenye majaribio ya chanjo ya awamu ya I/II nchini Marekani, Ulaya na Afrika. Chanjo imeonyesha usalama na uwezo kushawishi mwitikio wa kinga. Kisayansi haiwezekani kupata maambukizi ya VVU kutoka kwenye chanjo ambazo zilitumika katika utafiti huu.

Kundi la kufuatilia Usalama wa Jaribio la PrEPVacc hukagua taarifa za usalama za washiriki mara mbili kwa mwezi na huzingatia matukio au madhara yoyote ambayo yanaweza kutokea wakati washiriki wakiwa kwenye jaribio. Kundi la Usalama la Jaribio halijawa na wasiwasi wowote kuhusu madhara ya chanjo zilizojaribiwa katika utafiti wa PrEPVacc.

Washiriki wa PrEPVacc kusaidiwa katika upimaji na ushauri unaoendelea

Wakati wa jaribio, ushauri nasaha, ukuzaji na utoaji wa dawakinga ulisisitizwa katika kila hudhurio kwa washiriki wote, pamoja na ufuatiliaji wa kina kuhusu matumizi. Washiriki wote sasa wamekamilisha mahudhurio ya utafiti na wamepokea ushauri nasaha juu ya njia nyingine za kuzuia VVU zinazojulikana kuwa bora.

Upimaji wa ufuatiliaji wa VVU tayari unapatikana kupitia vituo, na PrEPVacc itaendelea kutoa ushauri nasaha na kukuza matumizi ya dawakinga na kuwezesha rufaa kwa ajili ya matibabu iwapo kuna maambukizi. Rufaa ya kupata huduma imewezeshwa kwa wale ambao wamepata VVU.

Wakati wa kutoka kwenye utafiti, takriban robo ya washiriki waliokuwa kwenye kundi la chanjo walionyesha ushahidi wa fingomwili inayotokana na Chanjo. Hali hii inayotambulika kama “VISP” hutokea wakati mwili umetoa fingomwili baada ya kupokea chanjo ya VVU, na matokeo ya baadaye ya vipimo vya VVU yanaweza kuonyesha hali ya maambukizi hata kama mtu hajaambukizwa VVU.

PrEPVacc daima ina nia ya kutoa huduma kwa washiriki wenye VISP ili kuhakikisha wanapata uchunguzi sahihi, na itafuatilia washiriki wote, kwa lengo la kufanya upimaji wa VVU mara mbili kwa mwaka kwa angalau miaka miwili ili kufuatilia mwenendo wa maambukizi, na kusaidia upatikanaji wa huduma na dawakinga.

Maoni kutoka kwa viongozi wa majaribio, wanajamii na mtaalamu huru

Mkurugenzi wa Jaribio la PrEPVacc, Dk Eugene Ruzagira, kutoka Kitengo cha Utafiti cha MRC/UVRI & LSHTM nchini Uganda, ambaye aliwasilisha matokeo kwenye mkutano wa UKIMWI 2024, alisema:

"Katika utafiti wa PrEPVacc, tumeweka washiriki wetu na jamii zao mbele na kuhakikisha usalama wao. Tulisimamisha majaribio ya chanjo mnamo Novemba 2023 mara tu tulipokuwa na ushahidi kwamba chanjo zisingeweza kuonyeshwa ufanisi. Tutaendelea kusaidia washiriki wetu kwa kutoa ushauri nasaha, huduma ya upimaji na upatikanaji wa huduma zilizopo za kujikinga na maambukizi.

“Kujitolea kwa washiriki wetu katika utafiti huu kumekuwa mfano wa kuigwa. Wao na jamii zao wanapaswa kujivunia juhudi zao na michango yao muhimu katika juhudi za kimataifa za kuzuia VVU.

"Taarifa za uhakika kwa jamii zetu ni kwamba ushauri nasaha wa mara kwa mara wa kupunguza hatari ya kupata maambukizi na matumizi ya zana zilizothibitishwa za kuzuia VVU huwasaidia watu kukabiliana vizuri na hatari ya kupata maambukizi. Idadi ya maambukizi mapya imepungua katika muda wote wa miaka sita ambayo tumekuwa tukifuatilia matukio ya VVU katika kila jamii ilioshiriki utafiti.”

“Tunaweza kujivunia juhudi ambazo tumefanya kukuza uwezo kupitia utafiti wa PrEPVacc ambazo zimewezesha ushiriki wetu katika muungano wa “BRILLIANT”. Muungano huu unajengwa juu ya urithi wa uongozi wa PrEPVacc Afrika katika utafiti wa kuzuia VVU.

"Tunatazamia matokeo kutoka kwenye utafiti jumuishi wa sayansi ya jamii wa PrEPVacc na matokeo ya utafiti wa dawakinga ndani ya utafiti wa PrEPVacc yatakayotolewa baadaye mwaka huu."

Profesa Sheena McCormack, Kiongozi wa utafiti wa PrEPVacc aliye katika kitengo cha majaribio ya tiba cha Baraza la Utafiti wa Matibabu katika Chuo Kikuu cha London, Uingereza, alisema:

"Siku zote unaingia kwenye utafiti na swali la kujibu ukiwa na fikira huru, lakini kuona kutolingana kwa hali za maambukizi kati ya kundi la chanjo na la kiponzaungo lilikuwa jambo la kushangaza na ambalo hatuwezi kuelezea. Tunadhani kuwa ni bahati tu lakini hatuwezi kuondoa uwezekano wa matokeo yake, kwa hivyo ni wazi tunahitaji kuendelea kuwaunga mkono washiriki na kutoa huduma ya upimaji wa VVU ili kufuatilia mwenendo huo.”

"Jumla ya idadi ya maambukizi katika jaribio ilikuwa ndogo zaidi kuliko tulivyotarajia, ambayo ni habari njema, hii inaakisi kile kinachotokea katika jamii pana. Tulikuwa tumeona kupungua kwa maambukizi kutoka mwaka 2018 katika Kundi la utafiti/washiriki wa Usajili, lakini hata hivyo, kiwango cha matukio ya maambukizi katika kundi la kipozaungo kilikuwa cha chini sana. Kwa kuwa hii inaathiri matokeo ya chanjo zote mbili inaongeza hali yetu ya kutokuwa na uhakika katika ulinganisho wa Makundi ya chanjo na kipozaungo.”

Mtafiti Mkuu wa PrEPVacc, Profesa Pontiano Kaleebu, aliyeko katika Kitengo cha Utafiti cha MRC/UVRI & LSHTM nchini Uganda, alisema:

"Maswali ya chanjo yaliyoulizwa katika jaribio yamejibiwa. Tunachosema wazi ni kwamba chanjo hizi hazitatolewa tena.”

"Tunahitaji uchunguzi zaidi wa chanjo ili kuelewa matokeo yetu, na ambayo inaweza kutumika kufahamisha muundo wa chanjo ya siku zijazo.”

“Matokeo yamekuwa ya kushangaza, na yamekuwa ya kukatisha tamaa. Lakini hiyo ni sayansi. Umekuwa utafiti mzuri sana, unaofuata viwango vya juu zaidi vya kimataifa. Sasa, lazima tusonge mbele kwa sababu ulimwengu unahitaji kuwa na chaguo katika zana za kuzuia VVU. Chanjo dhidi ya VVU inabaki kuwa sehemu inayotafutwa sana na muhimu katika sanduku la zana dhidi ya VVU."

Profesa Jonathan Weber Mfadhili wa PrEPVacc kutoka Chuo Kikuu cha London, Uingereza, alisema:

"Katika kipindi cha utafiti, imekuwa vizuri sana kuona idadi ya maambukizi mapya ikipungua katika jamii zote ambazo tumekuwa tukifanya nazo kazi. Utafiti wetu uliundwa vizuri sana, ukihusisha washiriki wachache iwezekanavyo na idadi ya chini ya maambukizi kujibu swali la ufanisi wa chanjo.

"Ninawashukuru wafanyakazi wote wanaofanya kazi kwa bidii katika kila kituo ambao wamewasilisha jaribio hili kwenye jamii, washiriki kwa kujitolea kwao bila kuchoka katika kuzuia VVU, na wanajamii ambao wametuongoza na kutuunga mkono sote katika utafiti. Ninashukuru sana mashirika ya kitaifa na mashirika ya kimataifa ambayo yamesaidia PrEPVacc katika safari yake yote na wametupa usaidizi na mwongozo wa hali ya juu.

"Ingawa ni wazi kwamba chanjo hazileti matokeo ya kinga, tunakabiliwa na matokeo haya yasiyotarajiwa katika kundi la kipozaungo, ambapo kuna matukio ya chini sana ya maambukizi ya VVU yanapingana na matukio yanayopatikana katika Kundi letu la usajili wa washiriki. Tunahitaji kungoja matokeo ya majaribio zaidi ili kuelewa jinsi seti hii ya matokeo ya kushangaza ilivyotokea, ikiwa sio kwa bahati pekee.

Xoliswa Nomvungu, Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Jamii kutoka kituo cha SAMRC Verulam, huko Durban, Afrika Kusini, alisema:

"Utafiti unaweka wazi kuwa ushiriki wa jamii ni muhimu katika awamu zote za utafiti. Katika jaribio la PrEPVacc kumekuwa na mwingiliano chanya wa jamii ili watu wafahamishwe vyema kuhusu maendeleo, matarajio, na uwazi. Ujumbe muhimu wa kupeleka nyumbani kutoka PrEPVacc ni kwamba matumizi thabiti ya dawakinga yanaweza kumzuia mtu kupata virusi vya UKIMWI."

Dk Peter Gilbert, Mtafiti Mkuu, Kituo cha Usimamizi wa Takwimu na Data cha HVTN (SDMC), ambaye ni mtu huru kwenye utafiti wa PrEPVacc na hana uhusiano nao, alisema:

"Kwa kuzingatia matokeo ya PrEPVacc kwamba makadirio ya viwango vya upatikanaji wa VVU-1 vilikuwa vya juu katika kundi la chanjo kuliko kipozaungo, ni muhimu kutathmini kwa kina na kuwasilisha ushahidi unaopatikana kuhusu kama chanjo kweli ziliongeza hatari au, vinginevyo, bila kutegemea mabadiliko ya takwimu yalitokea na chanjo zilikuwa salama kweli?”

"Kuziba pengo hili, nilifanya uchambuzi wa “Bayesian” ambao unatoa majibu kulingana na tafsiri hii niliyotaka, ambapo nilitumia njia ile ile niliyotumia hapo awali kwa majaribio mengine ya ufanisi wa chanjo ya VVU. Matokeo yake yalikuwa kwamba, kwa kila chanjo, kuna uwezekano wa 50-50 kwamba chanjo iliongeza hali ya hatari, dhidi ya chanjo ilikuwa salama, kama mchanganyiko wa matokeo juu ya njia nyingi za kufanya uchanganuzi, muhimu zaidi ni kuzingatia usambazaji tofauti wa hapo awali kwa ufanisi wa chanjo."

Ukweli wa haraka kuhusu PrEPVacc:

·        PrEPVacc ni utafiti wa kuzuia VVU unaoongozwa na Waafrika unaoungwa mkono na Umoja wa ulaya ambao, kwa mara ya kwanza, unafanya tathmini ya chanjo za VVU na kinga ya kabla ya kuambukizwa yani dawakinga kwa wakati mmoja.

·        PrEPVacc ilisajili zaidi ya watu 1,500 wenye umri kati ya miaka 18 na 40 katika vituo vinne vya majaribio nchini Uganda, Tanzania, na Afrika Kusini.

·        Maandalizi ya jaribio yalijumuisha Kundi la Usajili (utafiti wa uchunguzi), ambalo washiriki wake wa kwanza walisajiliwa Julai 2018.

·        Washiriki wa kwanza katika jaribio la chanjo walijiandikisha Desemba 2020, na mwisho Machi 2023. Washiriki wote walikuwa wametoka kwenye utafiti kufikia Juni 2024.

·        Wakati wa pendekezo la” IDMC” mnamo Novemba 2023, PrEPVacc ilikuwa jaribio pekee lililosalia la ufanisi wa chanjo ya VVU duniani.

·        Sehemu muhimu ya mradi wa PrEPVacc na jinsi unavyopangwa ni kukuza uwezo wa vituo vya Kiafrika kufanya majaribio ya baadaye vyenyewe na kukuza viongozi wa tafiti wa siku zijazo.

·        PrEPVacc inaongozwa na watafiti wa Kiafrika kutoka Entebbe nchini Uganda katika Kitengo cha Utafiti cha MRC/UVRI na LSHTM Uganda. Wanaungwa mkono na mashirika 15 washirika, sita kutoka Afrika, sita kutoka Ulaya na matatu kutoka Marekani. Mfadhili wa PrEPVacc ni Imperial College London. Tazama Vidokezo kwa Wahariri (2) kwa orodha kamili ya washirika.

·        Utafiti wa PrEPVacc unafadhiliwa na Ushirikiano wa Majaribio ya magonjwa ya binadamu ya Nchi za Ulaya na Nchi Zinazoendelea (EDCTP) kama sehemu ya Mpango wa EDCTP2 unaoungwa mkono na Umoja wa Ulaya. Tazama Madokezo kwa Wahariri (3) kwa orodha kamili ya wafadhili.

Wakati wa awamu ya kuandikisha na kusajili, toleo la video la uhuishaji wa fomu ya taarifa ya mshiriki lilitumiwa kuelezea utafiti kwa washiriki. Video hii inapatikana https://youtu.be/zHYC6SKKobc

Tovuti ya PrEPVacc:www.prepvacc.org

-mwisho-

 

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Tom Miller, Kiongozi wa Mawasiliano na Usambazaji wa matokeo ya PrEPVacc,prepvacc@gmail.com

Masaka, Uganda

Benson Muhumuza, Afisa Mawasiliano na Ushirikiano, MRC/UVRI na Kitengo cha Utafiti cha LSTM Uganda,benson.muhumuza@mrcuganda.org/mawasiliano@mrcuganda.org

Mbeya, Tanzania

Doreen Pamba, Mkuu wa Sayansi ya Jamii na Ushirikiano wa Jamii, Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya binadamu cha Mbeya (NIMR-Mbeya),dpamba@nimr-mmrc.org

Dar es Salaam, Tanzania

Helen Mtui, Kaimu Mkuu, Kitengo cha Mawasiliano na Masoko, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS),hmtui@muhas.ac.tz

Durban, Afrika Kusini

Tendani Tsedu, Mkuu wa Mawasiliano ya Biashara na Masoko, Baraza la Utafiti wa Magonjwa ya binadamu la Afrika Kusini,tendani.tsedu@mrc.ac.za

Yolanda Phakela, Meneja wa PR, Baraza la Utafiti wa Magonjwa ya binadamu la Afrika Kusini,yolanda.phakela@mrc.ac.za

Vidokezo kwa Wahariri

(1) Wasilisho la mukhtasari kwenye kongamano la UKIMWI 2024: OAC08 Matokeo ya mwisho ya ufanisi wa chanjo kutoka kwenye utafiti wa PrEPVacc: Majaribio ya chanjo ya kuzuia VVU ya awamu ya IIb ya dawa mbili amilifu kila moja ikilinganishwa na kipozaungo. Eugene Ruzagira | 23 Julai 2024 | 16:30-17:30 | Ukumbi B0/Chaneli 4 (https://programme.aids2024.org/Programme/Session/207 | *PPT*)

(2) Washirika wa PrEPVacc

Nyuma ya PrEPVacc kuna watafiti wa ngazi ya juu 80, matabibu, wanasayansi ya jamii, wataalamu wa mawasiliano ya jamii na majukumu ya usaidizi wa kitaalamu, kutoka kwa mashirika 15 washirika. Wana uzoefu wa kina wa kufanya kazi za VVU na magonjwa mengine ya kuambukiza, pamoja na majaribio ya tiba, hasa katika majaribio ya chanjo ya VVU na dawakinga kote Ulaya na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

·        Baraza la Utafiti wa Tiba / Taasisi ya Utafiti wa Virusi ya Uganda na Shule ya Usafi na Magonjwa ya Kitropiki ya London Kitengo cha Utafiti cha Uganda, Uganda

·        Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Tanzania

·        Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa magonjwa ya binadamu - Kituo cha Mbeya, Tanzania

·        Kitengo cha Utafiti wa VVU na Magonjwa mengine ya Kuambukiza, “MRC” cha Afrika Kusini, Afrika Kusini

·        Chuo cha Imperial London, Uingereza

·        Baraza la Utafiti wa Tiba Kitengo cha Majaribio katika Chuo Kikuu cha London, Uingereza

·        Kituo cha chou kikuu cha VAUD, Uswisi

·        Taasisi ya Karolinska, Uswidi

·        Kituo cha Tiba, Chuo Kikuu cha Munich (LMU), Ujerumani

·        Mpango wa Kimataifa wa Chanjo ya UKIMWI (IAVI)

·        Taasisi ya Utafiti wa Afya Afrika

·        Msingi wa “EuroVacc”

·        Gilead Sciences, Inc

·        Ufumbuzi wa Kimataifa kwa Magonjwa ya Kuambukiza

·        Shule ya Tiba ya Virginia Mashariki, CONRAD, Marekani

·        Mpango wa Utafiti wa VVU wa Kijeshi katika Taasisi ya Utafiti ya Jeshi la Walter Reed (WRAIR)

https://www.prepvacc.org/partners

 

(3) Wafadhili wa PrEPVacc

PrEPVacc ni ushirikiano wa umma na binafsi. Ushirikiano wa Majaribio ya Tiba ya Nchi za Ulaya na Nchi Zinazoendelea (EDCTP) ulitoa ruzuku ya €15M kwa ajili ya utafiti huo na washirika wote wa taasisi wanatoa ufadhili wa pamoja kupitia mishahara ya wafanyakazi. “Gilead Sciences, Inc” inatoa msaada kwa mradi huo kupitia vifaa, dawa, na ufadhili. PrEPVacc pia inaungwa mkono na mashirika mbalimbali kama USAID na PEPFAR, USMHRP, SVRI, SAMRC, UKRI Medical Research Council, Wellcome Trust, Bill and Melinda Gates Foundation, SIDA, na Bundesministerium für Bildung und Forschung (BMBF).

 

https://www.prepvacc.org/funders

MUHAS, NIMR-MMRCPrEP Vacc